Sheria na Masharti ya Ziada ya Hifadhi ya Google

Tarehe ya kuanza kutumika: 31 Machi, 2020 (angalia toleo la awali)

Ili uweze kutumia Hifadhi ya Google, ni lazima ukubali (1) Sheria na Masharti ya Google na (2) Sheria na Masharti haya ya Ziada ya Hifadhi ya Google (“Sheria na Masharti ya Ziada ya Hifadhi ya Google”).

Tafadhali soma kila mojawapo ya hati hizi kwa umakini. Kwa pamoja, hati hizi zinafahamika kama “Sheria na Masharti”. Zinabainisha mambo unayoweza kutarajia kutoka kwetu unapotumia huduma zetu na mambo tunayotarajia kutoka kwako.

Ingawa si sehemu ya Sheria na Masharti haya, tunakuhimiza usome Sera yetu ya Faragha ili uelewe kwa njia bora jinsi unavyoweza kusasisha, kudhibiti, kutuma na kufuta taarifa zako.

1. Maudhui Yako

Hifadhi ya Google inakuruhusu kupakia, kuwasilisha, kuhifadhi, kutuma au kupokea maudhui. Kama ilivyobainishwa katika Sheria na Masharti ya Google, maudhui yako husalia kuwa yako. Hatudai umiliki katika maudhui yako yoyote, ikiwemo maandishi, data, taarifa na faili zozote unazopakia, unazoshiriki au unazoweka katika akaunti yako ya Hifadhi. Sheria na Masharti ya Google huipa Google leseni kwa madhumuni tu ya kuendesha na kuboreshsa huduma za Hifadhi ya Google — kwa hivyo ukiamua kushiriki hati na mtu mwingine, au ukitaka kuifungua kwenye kifaa tofauti, tunaweza kukupa kipengele kinachofanya hivyo.

Hifadhi ya Google pia hukuruhusu kushirikiana na watumiaji wengine wa Hifadhi ya Google kwenye maudhui yao. “Mmiliki” wa maudhui ndiye anayedhibiti maudhui hayo na jinsi yanavyotumiwa.

Mipangilio ya kushiriki iliyo katika Hifadhi ya Google inakuwezesha kudhibiti kile ambacho watu wengine wanaweza kufanyia maudhui yako katika Hifadhi ya Google. Mipangilio ya faragha ya faili zako inategemea folda au hifadhi zilipowekwa. Faili zilizo katika hifadhi yako binafsi ni za faragha isipokuwa ukiamua kuzishiriki. Unaweza kushiriki maudhui yako na unaweza kuwapa watumiaji wengine udhibiti wa maudhui yako. Faili unazounda au kuweka katika folda au hifadhi unazotumia pamoja na wengine zitarithi mipangilio ya kushiriki na huenda zikarithi mipangilio ya umiliki ya folda au hifadhi zilipowekwa. Hatutashiriki faili wala data yako na wengine isipokuwa kwa mujibu wa Sera yetu ya Faragha.

Hatutatumia maudhui yako kwa ajili ya kampeni za uuzaji au utangazaji.

2. Sera za Mpango

Tunaweza kutathmini maudhui ili kubainisha kama hayatii sheria au yanakiuka Sera zetu za Mpango na tunaweza kuondoa au kukataa kuonyesha maudhui ambayo tunaamini kwamba yanakiuka sera zetu au sheria. Lakini hilo halimaanishi moja kwa moja kwamba tunakagua maudhui, kwa hivyo tafadhali usichukulie tu kwamba tunafanya hivyo.