Sheria na Masharti ya Hifadhi ya Google

Mara ya mwisho kubadilishwa ni Tarehe 10 Desemba, 2018 Tarehe ya Kuanza kutumika: 22 Januari, 2019

1. Utangulizi

Asante kwa kutumia Hifadhi ya Google. Hifadhi ya Google ni Huduma inayotolewa na Google LLC (“Google” au “sisi”), iliyo na makao yake makuu katika 1600 Amphitheatre Parkway, Mountain View California 94043, Marekani. Ikiwa unaishi nchini Uswisi au katika nchi washirika katika Makubaliano ya Kiuchumi ya Ulaya, Hifadhi ya Google inatolewa na Google Ireland Limited (“Google” au “sisi”), kampuni iliyosajiliwa na inayofanya kazi chini ya sheria za Ayalandi (Nambari ya Usajili: 368047) na iliyo na makao yake katika Gordon House, Barrow Street, Dublin 4, Ayalandi. Sheria na Masharti haya ya Hifadhi ya Google (ambayo tunayaita “Masharti”) yanasimamia matumizi na ufikiaji wako wa Hifadhi ya Google na maudhui yako yaliyo katika Hifadhi ya Google. Sera yetu ya Faragha inaeleza jinsi tunavyokusanya na kutumia maelezo yako, ilhali Sera zetu za Mpango zinatoa muhtasari wa wajibu wako unapotumia Huduma yetu.

Matumizi yako ya Hifadhi ya Google yanahitaji ukubali Masharti haya. Tafadhali yasome kwa makini. Kama huelewi Masharti haya, au hukubaliani na sehemu yake yoyote, basi hufai kutumia Hifadhi ya Google.

2. Matumizi yako ya Hifadhi ya Google

Masharti ya Umri. Ili uweze kutumia Hifadhi ya Google, ni lazima uwe umri wa miaka 13 au zaidi. Kama una umri wa angalau miaka 13 lakini hujatimiza umri wa miaka 18, ni lazima uwe na ruhusa ya mzazi au mlezi wako wa kisheria ili uweze kutumia Hifadhi ya Google na kukubali Masharti.

Matumizi ya Binafsi. Kwa kukubali masharti haya, unakubali kutotumia Hifadhi ya Google kwa makusudi ya biashara; ni sharti utumie huduma ya Hifadhi ya Google kwa makusudi ya binafsi yasiyo ya biashara. Tunapendekeza biashara zitumie GSuite.

Akaunti Yako ya Google. Utahitaji Akaunti ya Google ili uweze kutumia Hifadhi ya Google. Ili kulinda Akaunti yako ya Google, usifichue nenosiri lako. Unawajibika kwa shughuli zinazofanyika kwenye au kupitia Akaunti yako ya Google. Jaribu kutotumia nenosiri lako la Akaunti ya Google kwenye programu zinazotolewa na wahusika wengine. Ukitambua matumizi yoyote ambayo hayajaidhinishwa ya nenosiri lako au Akaunti ya Google, fuata maagizo haya.

Maadili Yako. Usitumie Hifadhi ya Google vibaya. Unaweza tu kutumia Hifadhi ya Google kama inavyoruhusiwa na sheria, pamoja na sheria na kanuni zinazotumika za kudhibiti uuzaji wa bidhaa zilizotengenezwa nchini na zilizoagizwa kutoka nje kwa nchi nyingine. Unawajibikia unachofanya na maudhui yako yaliyohifadhiwa katika Hifadhi ya Google na lazima utii Sera zetu za Mpango. Tunaweza kutathmini maadili na maudhui yako yaliyo katika Hifadhi ya Google kuona kama yanatii Masharti na Sera zetu za Mpango.

Hifadhi ya Google inapatikana kwenye vifaa vya mkononi. Usitumie Hifadhi ya Google kwa njia ambayo inakuvuruga mawazo na kukuzuia kutii sheria za barabarani au za usalama.

Maudhui Yako Hifadhi ya Google inakuruhusu kupakia, kuwasilisha, kuhifadhi, kutuma au kupokea maudhui. Haki zozote za uvumbuzi ulizo nazo katika maudhui hayo zinabaki kuwa zako. Kwa ufupi, kilicho chako kinabaki kuwa chako.

Unapopakia, kuwasilisha, kuhifadhi, kutuma au kupokea maudhui kwenye au kupitia Hifadhi ya Google, unaipa Google leseni duniani kote ya kutumia, kupangisha, kuhifadhi, kurudufisha, kubadilisha, kuunda kazi nyingine zinazoiga maelezo msingi (kama zile zinazotokana na kutafsiri, marekebisho au mabadiliko mengine tunayoyafanya ili maudhui yako yafanye kazi vyema zaidi na Huduma zetu), kuwasilisha, kuchapisha, kucheza hadharani, kuonyesha hadharani na kusambaza maudhui kama hayo. Haki unazotoa katika leseni hii ni kwa madhumuni tu ya kuendesha, kutangaza na kuboresha Huduma zetu na kubuni nyingine mpya. Leseni hii itaendelea kuwepo hata kama utaacha kutumia Huduma zetu isipokuwa kama utafuta maudhui yako. Hakikisha kwamba una haki zinazohitajika kutupa leseni hii kwa ajili ya maudhui yoyote unayowasilisha kwenye Hifadhi ya Google.

Mipangilio ya Kushiriki iliyo katika Hifadhi ya Google inakuwezesha kudhibiti kile ambacho watu wengine wanaweza kufanyia maudhui yako katika Hifadhi ya Google. Kwa chaguo-msingi, mipangilio hiyo hukufanya uwe mdhibiti wa maudhui yote unayounda au kupakia kwenye Hifadhi ya Google. Unaweza kushiriki maudhui na unaweza kuwapa watumiaji wengine udhibiti wa maudhui yako.

Mifumo yetu ya kiotomatiki huchanganua maudhui yako ili kukupa vipengele vya bidhaa vinavyokufaa wewe binafsi, kama vile matokeo ya utafutaji yanayokulenga binafsi na ugunduzi wa barua taka na programu hasidi. Uchanganuzi huu hufanyika wakati maudhui yanapokewa, kushirikiwa, kupakiwa na wakati yanahifadhiwa. Unaweza kupata maelezo zaidi kuhusu jinsi Google inavyotumia na kuhifadhi maudhui katika Sera ya Faragha. Ukiwasilisha maoni au mapendekezo kuhusu Hifadhi ya Google, huenda tukatumia maoni au mapendekezo yako bila ya kuwa na wajibu kwako.

Matangazo Kuhusiana na matumizi yako ya Hifadhi ya Google, tunaweza kukutumia matangazo ya huduma, ujumbe wa usimamizi na maelezo mengine. Unaweza kujiondoa ili usipokee baadhi ya mawasiliano hayo.

Huduma zetu za Hifadhi ya Google. Kutumia Hifadhi ya Google hakukupi umiliki wa haki zozote za uvumbuzi katika Hifadhi ya Google wala maudhui unayofikia. Huruhusiwi kutumia maudhui kutoka kwenye Hifadhi ya Google isipokuwa upate ruhusa ya anayeyamiliki au kama inakubaliwa vinginevyo na sheria. Masharti haya hayakupi haki ya kutumia chapa au nembo zozote zinazotumika katika Hifadhi ya Google. Usiondoe, usifiche wala usibadilishe ilani zozote za kisheria zinazoonyeshwa kwenye au pamoja na Hifadhi ya Google.

3. Ulinzi wa Faragha

Sera ya Faragha ya Google inaeleza jinsi tunavyoshughulikia data yako ya binafsi unapotumia Hifadhi ya Google. Kwa kutumia Hifadhi ya Google, unakubali kwamba Google inaweza kutumia data kama hiyo kulingana na sera zetu za faragha.

4. Ulinzi wa Hakimiliki

Huwa tunajibu taarifa za madai ya kukiuka hakimiliki na kufunga akaunti za wakiukaji wa kurudia kulingana na njia iliyowekwa katika Sheria ya Milenia ya Hakimilki Dijitali ya Marekani.

Huwa tunatoa maelezo ya kuwasaidia wenye hakimiliki kusimamia haki zao za uvumbuzi mtandaoni. Kama unadhani kuna mtu anayekiuka hakimiliki zako na unataka kutujulisha, unaweza kupata maelezo kuhusu jinsi ya kuwasilisha taarifa na sera ya Google kuhusu kujibu taarifa katika Kituo chetu cha Usaidizi.

5. Sera za Mpango

Tunaweza kutathmini maudhui ili kubainisha kama hayatii sheria au yanakiuka Sera zetu za Mpango na tunaweza kuondoa au kukataa kuonyesha yale ambayo tunaamini kwa haki kwamba yanakiuka sera au sheria zetu. Lakini hilo halimaanishi moja kwa moja kwamba tunakagua maudhui, kwa hivyo tafadhali usichukulie tu kwamba tunafanya hivyo.

6. Kuhusu Programu katika Huduma zetu

Programu Teja. Hifadhi ya Google inajumuisha programu teja inayoweza kupakuliwa (“Programu”). Programu hii inaweza kujisasisha kiotomatiki kwenye kifaa chako wakati toleo au kipengele kipya kinapopatikana. Google inakupa leseni ya binafsi, ya duniani kote, isiyo na mirabaha, isiyoweza kukabidhiwa mhusika mwingine na isiyo ya kipekee ya kutumia Programu inayotolewa kwako kama sehemu ya Hifadhi ya Google. Leseni hii ni ya makusudi tu ya kukuwezesha kutumia na kufurahia manufaa ya Hifadhi ya Google kama inavyotolewa na Google, kwa njia inayoruhusiwa na Masharti haya. Huruhusiwi kunakili, kubadilisha, kusambaza, kuuza wala kukodisha sehemu yoyote ya Hifadhi ya Google au programu zilizojumuishwa, isipokuwa kama sheria zinakataza vikwazo hivyo au tumekupa ruhusa iliyoandikwa.

Programu huria. Programu huria ni muhimu kwetu. Baadhi ya programu zinazotumika katika Hifadhi ya Google zinaweza kuwa zimetolewa kwa mujibu wa leseni ya programu huria tutakayokupa. Huenda pakawa na vipengele katika leseni ya programu huria ambavyo vinabatili baadhi ya Masharti haya.

7. Kubadilisha na Kukomesha Matumizi ya Hifadhi ya Google

Mabadiliko kwenye Hifadhi ya Google. Huwa tunabadilisha na kuboresha Hifadhi ya Google kila wakati. Tunaweza kuboresha utendakazi au usalama, kubadilisha zana au vipengele au kufanya mabadiliko ili kutii sheria au kuzuia shughuli zisizo halali kwenye, au matumizi mabaya ya mifumo yetu. Unaweza kujisajili ili uwe ukipokea maelezo kuhusu Hifadhi ya Google here. Tutakuarifu mapema kuhusu mabadiliko muhimu katika Hifadhi ya Google ambayo tunaamini kwa haki yataathiri vibaya matumizi yako ya Hifadhi ya Google. Hata hivyo, kuna nyakati ambapo tutahitaji kufanya mabadiliko kwenye Hifadhi ya Google bila kutoa taarifa. Hili litakuwa tu katika nyakati ambapo tunahitaji kuchukua hatua ili kuhakikisha usalama na utendakazi wa huduma, kuzuia matumizi mabaya au nyakati ambapo tunahitaji kuchukua hatua kutimiza matakwa ya sheria.

Kusimamisha na Kukomesha Matumizi. Unaweza kuacha kutumia Hifadhi ya Google wakati wowote ule, ijapokuwa tutasikitishwa na kuondoka kwako. Tunaweza kusimamisha au kukuzuia kufikia Hifadhi ya Google kabisa ukikiuka Sera zetu za Mpango. Tutakuarifu kabla ya kusimamisha au kukomesha uwezo wako wa kufikia Hifadhi ya Google. Hata hivyo tunaweza kusimamisha au kukomesha uwezo wako wa kufikia Hifadhi ya Google bila kukuarifu kama unatumia Hifadhi ya Google kwa njia inayoweza kutuletea dhima ya kisheria au kuvuruga uwezo wa watumiaji wengine kufikia na kutumia Hifadhi ya Google.

Kukomeshwa kwa Hifadhi ya Google. Tukiamua kukomesha huduma ya Hifadhi ya Google, tutakuarifu angalau siku 60 kabla ya kufanya hivyo. Katika muda huu, utakuwa na nafasi ya kuondoa faili zako kwenye Hifadhi ya Google. Baada ya muda huo wa siku 60, hutaweza kufikia faili zako. Tunaamini kwamba unamiliki faili zako na kwamba ni muhimu kulinda faili kama hizo. Kwa maelezo kuhusu jinsi ya kupakua faili zako, tafadhali tembelea ukurasa wetu wa usaidizi.

8. Kununua Nafasi ya Ziada ya Kuhifadhi na Malipo

Hifadhi Isiyolipishwa. Google inakuruhusu kutumia GB 15 za nafasi ya Google ya kuhifadhi mtandaoni bila kulipishwa (ikitegemea kutii kwako kwa Masharti haya), ambayo inaweza kutumiwa katika Hifadhi ya Google, Gmail na huduma ya Picha kwenye Google.

Nunua Nafasi ya Ziada ya Kuhifadhi. Unaweza pia kununua hifadhi ya ziada (“Hifadhi ya Kulipia”) ukiihitaji. Tutakutumia bili kiotomatiki kuanzia siku utakapohamia Hifadhi ya Kulipia na kila wakati kipindi cha huduma kinapoanza upya hadi wakati utakapoghairi. Lazima ukubali masharti ya kulipa yaliyobainishwa katika Masharti ya Google Payments. Kama huna akaunti ya Google Payments, unaweza kuifungua kwa kwenda kwenye kiungo hiki, ambapo pia utapata maelezo zaidi kuhusu Google Payments. Ilani ya faragha ya Google Payments pia inatumika kila unapotaka kununua Hifadhi ya Kulipia ukitumia akaunti ya Google Payments. Tafadhali hakikisha kuwa umesoma masharti hayo kwa makini kabla ya kununua chochote.

Kughairi. Hifadhi yako ya Kulipia itaendelea kufanya kazi hadi ighairiwe, ishushwe kiwango au ikomeshwe kwa mujibu wa Masharti haya. Unaweza kughairi au kushusha kiwango cha Hifadhi yako ya Kulipia wakati wowote ule katika mipangilio ya Hifadhi ya Google mipangilio ya hifadhi. Ukighairi au kushusha kiwango cha hifadhi, mabadiliko haya yatatumika katika kipindi kijacho cha kulipa baada ya kipindi cha huduma kilichopo kuisha. Usipolipia Hifadhi yako ya Kulipia kwa wakati unaofaa, tunabaki na haki ya kushusha kiwango cha akaunti yako na kupunguza nafasi yako ya kuhifadhi hadi kiwango kisicholipiwa. Tumetoa maelezo kuhusu mchakato wa kughairi na kurejeshewa fedha kwa ajili ya Hifadhi yako ya Kulipia katika sera yetu ya Kununua, Kughairi na Kurejeshewa Fedha.

Mabadiliko ya Hifadhi ya Kulipia na Bei. Tunaweza kubadilisha hifadhi ya kulipia na bei inayotumika lakini tutakuarifu kuhusu mabadiliko hayo kabla hayajatekelezwa. Mabadiliko hayo yataanza kutumika wakati muda wa mpango wa huduma unaotumia sasa utakwisha, wakati ujao wa kulipa baada ya taarifa. Tutakuarifu angalau siku 30 kabla ya kuongeza bei au kupunguza nafasi ya hifadhi ya kulipia. Ukipewa taarifa chini ya siku 30, mabadiliko hayatatekelezwa hadi baada ya wakati ujao wa kulipa. Kama hutaki kuendelea kutumia nafasi au bei mpya ya hifadhi ya kulipia, unaweza kughairi au kushusha kiwango cha Hifadhi yako ya Kulipia wakati wowote ule katika mipangilio ya hifadhi. Ukighairi au kushusha kiwango cha hifadhi, mabadiliko haya yatatumika katika kipindi kijacho cha kulipa baada ya kipindi cha huduma kilichopo kuisha; tutaendelea kukupa uwezo wa kufikia faili zako au kukupa nafasi ya kuondoa faili zako kwenye Hifadhi ya Google.

9. Dhima na Makanusho yetu

Tunatoa huduma ya Hifadhi ya Google kwa kiwango kizuri cha ujuzi na umakini na tunatumai utafurahia kutumia Hifadhi ya Google. Lakini kuna mambo fulani ambayo hatuahidi kuhusu Hifadhi ya Google. Isipokuwa kama imetajwa bayana, hatutoi ahadi yoyote kuhusu vipengele hasa vinavyopatikana kupitia Hifadhi ya Google, utegemeaji, upatikanaji au uwezo wake kutimiza mahitaji yako.

10. Dhima ya Hifadhi ya Google

Google na watoa huduma na wasambazaji wake hawawajibiki kisheria wala hawabebi dhima kwa ajili ya:

(a) hasara ambazo hazikusababishwa na sisi kukiuka Masharti haya;

(b) hasara au uharibifu wowote ambao kwa hakika, kufikia wakati wa kuratibisha mkataba husika, haungetokana na Google kukiuka Masharti haya; au

(c) hasara zinazohusiana na biashara yako yoyote, ikiwa ni pamoja na kupoteza faida, mapato, fursa au data.

Dhima ya jumla ya Google na watoa huduma na wasambazaji wake, kwa madai yoyote kwa mujibu wa masharti haya, ikiwa ni pamoja na dhima yoyote iliyodokezwa, ina kikomo cha idadi uliyotulipa kutumia huduma (au kama hoja ya dai ni huduma isiyolipishwa, cha kukupa huduma hizo tena).

Hakuna chochote katika masharti haya kinachonuiwa kuondoa au kuweka kikomo kwenye dhima ya Google na watoa huduma wake na wasambazaji wake, kukija masuala kama kifo au kuumia kwa mtu binafsi, ulaghai, uwasilishaji mbaya wa ulaghai au dhima yoyote ambayo haiwezi kuondolewa kisheria.

11. Sheria Zinazodhibiti Masharti Haya.

Kama unaishi nje ya nchi washirika katika Makubaliano ya Kiuchumi au nchini Uswisi, sheria za California, Marekani, ukiondoa kanuni za California za mgongano wa sheria, zitatumika katika mabishano yoyote yanayotokana au yanayohusiana na Masharti haya au Hifadhi ya Google. Madai yote yanayotokana au yanayohusiana na Masharti haya au Hifadhi ya Google yatashughulikiwa katika mahakama za nchi au za jimbo katika Kaunti ya Santa Clara, California, Marekani, na wewe na Google mnakubali kuwa chini ya mamlaka ya mahakama hizo kibinafsi.

Kama unaishi katika nchi washirika katika Makubaliano ya Kiuchumi au nchini Uswisi, sheria na mahakama za nchi unakoishi zitatumika katika mabishano yoyote yanayotokana au yanayohusiana na Masharti haya au Hifadhi ya Google na unaweza kuanzisha mashtaka katika mahakama za mahali ulipo. Mabishano yanaweza kuwasilishwa kwenye mfumo wa Tume ya Ulaya wa Kutatua Mabishano ili yatatuliwe mtandaoni.

12. Kuhusu Masharti haya

Tunaweza kubadilisha Masharti haya au masharti mengine ya ziada yanayotumika kwenye Hifadhi ya Google, kwa mfano: kuambatana na mabadiliko katika Hifadhi ya Google, sheria, desturi au sera za siasa au za uchumi; au kuitikia mwongozo wa asasi zinazotoa kanuni au mashirika husika ya sekta; au kuiwezesha Google kutimiza wajibu wake. Unafaa kuangalia Masharti haya mara kwa mara. Tutachapisha taarifa kuhusu mabadiliko yanayofanywa katika Masharti haya kwenye ukurasa huu (“Masharti ya Ziada”) katika Hifadhi ya Google na tutakuarifu kuhusu mabadiliko muhimu katika Masharti kabla hayajafanyika. Mabadiliko hayatatumika katika hali zilizopita na yataanza kutumika angalau siku 14 baada ya kuchapishwa au baada ya kukuarifu. Hata hivyo, mabadiliko yanayoshughulikia zana au vipengele vipya (“Huduma Mpya”) au mabadiliko yanayofanywa kwa sababu za kisheria yatatekelezwa mara moja. Kama hukubali masharti yaliyobadilishwa ya Huduma Mpya, unastahili kuacha kutumia Huduma hiyo Mpya (kwa maelezo zaidi, angalia "Kukomesha Matumizi" hapo juu).

Kama kuna ukinzani kati ya Masharti haya na Masharti ya Ziada, Masharti ya Ziada yatadhibiti ukinzani huo.

Masharti haya yanadhibiti uhusiano kati yako na Google. Hayatoi haki zozote kufaidi mtu mwingine.

Kama hutatii masharti haya na tusichukue hatua mara moja, haimaanishi kwamba tunasalimisha haki zozote tulizo nazo (kama vile kuchukua hatua baadaye).

Ikitokea kwamba sharti fulani haliwezi kutimizwa, hilo halitaathiri masharti mengine yoyote.

Kwa maelezo ya jinsi ya kuwasiliana na Google, tafadhali tembelea ukurasa wetu wa mawasiliano.